Waziri Mchengerwa atoa wito kwa jeshi kuwa na timu ya soka.

 

Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ametoa wito  kwa majeshi kuanzisha  timu  ya soka itakayoshiriki ligi kuu nchini ili kuongeza ushindani na mvuto wa ligi.

Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo usiku wa kuamkia leo Agosti 28, 2022 kwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jakob John Mkunda katika uwanja wa Gofu wa jeshi wa Lugalo jijini Dar es Salaam wakati akifunga  mashindano ya Gofu ya NBC Lugalo Patron Trophy 2022.

Amefafanua kuwa majeshi yamekuwa na historia ya kutoa mchango mkubwa ambapo ameelezea kwamba   wachezaji wengi wanaoshinda katika mashindano mengi wanatoka kwenye majeshi.

Aidha amesema kutokana na nidhamu iliyojengeka kwenye majeshi anaimani kuwa jeshi linauwezo wa kuanzisha timu hiyo ambayo itakuwa miongoni mwa timu tishio ndani na nje ya nchi yetu.

Amesifu juhudi zinafanywa na jeshi katika kuanzisha klabu ya gofu na  miundombinu ya michezo huo Dar es Salaam na Dodoma na kuruhusu raia kutumia ambapo ameeleza kuwa kufanya hivyo kunakuza mchezo huo.

Ametoa wito kwa watu wengine kushiriki kwenye mashindano hayo na kusisitiza kuwa katika mashindano yanayofuata yeye pia atashiriki.

Aidha,  ametumia tukio hilo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi makubwa anayoyafanya kwenye michezo na hatimaye kupata mafanikio makubwa kwenye michezo katika kipindi kifupi cha Serikali yake.

Akitolea mfano amesema Tanzania  haikuwahi kupata medali katika mashindano ya Jumuiya ya Madola toka mwaka 1982 ambapo katika kipindi cha  mwaka huu imefanikiwa kutwaa medali tatu.

Katika tukio hilo mlezi wa timu ya gofu ya Lugalo, Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo amekabidhi ulezi wa timu hiyo kwa Mkuu wa Majeshi wa sasa Jenerali Jakob John Mkunda.

Mwanzilishi wa Klabu Gofu ya Lugalo, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali, George Waitara  amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Afande Mabeyo na kuekeza kuwa ana imani kubwa na mlezi mpya wa klabu hiyo Jenerali Mkunda kwa kuwa amekuwa mlezi wa wachezaji wengi wa majeshi ambao ndiyo wanaong'aa kwenye mashindano ya kimataifa hivi sasa.

Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu ya Lugalo, Brigedia Jenerali mstaafu Michael Luwongo amemwomba Waziri Mchengerwa kuona uwezekano wa kuwa kitengo maalum cha mchezo wa Gofu katika Wizara yake ili kuuinua mchezo huo kama michezo mingine ya kimkakati.

Katika tukio hilo Mhe. Mchengerwa ambaye alikuwa mgeni rasmi alitoa zawadi kwa washindi wote ambapo ameeleza kuwa  washiri wote ni washindi, na kuwataka walioshindwa kutokata tamaa na badala yake kuongeza bidii ili hatimaye washinde.

Vikundi mbalimbali vya majeshi vya muziki vilipamba tukio hilo kwa burudani nzuri huku wageni wakivutunza vikundi hivyo na kushiriki kucheza pamoja.


Comments

Popular posts from this blog

VIONGOZI WA DINI MKOANI SINGIDA WAJA NA MAAZIMIO SABA UCHAGUZI MKUU

Wadau wapongeza MIF kwa kusaidia mtoto wa kike Zanzibar, wajitokeza kuichangia

Hongereni Simba- Mhe, Mchengerwa